Watoto ni malaika wa kweli wanaoweza kutufundisha jinsi ya kuishi maisha mazuri. Ingawa wakati mwingine hawatambui wanachokuwa wakikifanya, lakini wanatupa nafasi ya kujifunza vitu vingi ambavyo tunavisahau tunapokuwa watu wazima.
Kuna sababu ya kwanini watoto wanaitwa zawadi kutoka kwa Mungu. Wanatufundisha kuboresha maisha yetu, kuona vitu vizuri kwenye maisha pamoja na kujaa tabasamu kila siku. Ni wazi kuwa yapo mambo mengi mazuri na yenye manufaa makubwa ambayo kila mtu anaweza kujifunza kutoka kwa watoto; yafahamu mambo hayo sasa.
Kuwa na Furaha
Maisha ya watoto yamejaa furaha. Mara nyingi utawakuta watoto wakiimba, wakikimbia, wakiruka, wakitaniana kwa furaha bila wasiwasi. Hili limefanya maisha ya utoto kuwa sawa na kito cha thamani. Jambo hili ni tofauti na watu wazima, kwani wao huwaza na kuhangaikia mengi huku wakiwa hawana furaha. Hali hii hufanya maisha ya watu wengi kukosa ladha na tija. Ni muhimu kujifunza kuwa na furaha kama watoto ili uweze kuwa na tija zaidi.
Kuheshimu Hisia Zako
Mtoto akiwa na hasira ataonyesha, akitaka kulia atalia, akiwa na furaha pia ataonyesha. Halii hi ni kinyume kwa watu wazima kwani wao wanaweza kuwa wanacheka lakini moyoni wanalia; au wanalia kumbe moyoni wanacheka. Ni vyema ukafahamu umuhimu wa kuheshimu hisia zako; usibebe uchungu ndani ya moyo wako. Kama unahuzuni basi itoe, kama unafuraha pia ionyeshe furaha yako
Upendo wa Kweli
Upendo ulioko kwa watoto ni wakushangaza. Mtoto atamjali mwenzake kama yeye mwenyewe. Mtoto anapopata zawadi au kitu fulani, ni wazi atatamani kugawana au kukitumia na marafiki zake. Hali ni tofauti kwenye maisha ya watu wazima kwani maisha yao yamejaa ubinafsi, choyo na chuki zisizokuwa na sababu. Jifunze kuwa na upendo kama wa mtoto; upendo siyo vitu bali ni moyo uliyo tayari.
Kuwa na Ndoto Kubwa
Ninapenda sana kusikiliza mawazo na ndoto za watoto. Mara huyu anataka kuwa rubani, huyu raisi, huyu daktari n.k. Ni ukweli usiopingika kuwa kadri unavyowaza mawazo makubwa ndivyo unavyoongeza nafasi yako ya kuwa na mafanikio makubwa. Jiulize kama mtoto hana msingi wowote lakini anawaza ndoto kubwa kwanini wewe mtu mzima uwaze ndoto ndogo?
Kukubali kuwa haufahamu kila kitu
Kama nilivyoeleza juu ya mtoto kuwa mkweli, pia mtoto yuko tayari kujifunza na kusema hafahamu. Kama kweli mtoto hakifahamu kitu, yupo tayari kusema hakifahamu. Ni vyema watu wazima kujifunza kuwa hawajui kila kitu kuliko kutarazia mambo kwa kujifanya wajuaji na mwishoni wakaharibu.
haya ni baadhi ya yale mengi ambayo tunaweza kujifunza kutoka kwa watoto wetu, pia unaweza kuongezea yale mengi ambayo hatujayasema na kutushirikisha.
jisikie huru kuwa mmoja kati ya wale tunaotamani kujifunza kutoka kwa watu bila kujali namna walivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here